Saturday, July 30, 2011

Kesi mpaka Muhimbili.


HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili (MNH), imegeuka kuwa mahakama kwa muda baada ya dereva wa Kampuni ya Mabasi ya Hood Ltd, Saleh Tembo (42), kusomewa mashtaka 23, chini ya ulinzi kwenye hospitali hiyo.
Tembo anadaiwa kusababisha ajali hivi karibuni iliyopoteza maisha ya watu sita na wengine 17, kujeruhiwa amelazwa wodi namba 17 Sewahaji kwa matibabu, baada ya kuvunjika mguu na mbavu.


Katika ajali hiyo, basi hilo liligongana na lori la mafuta na kusababisha magari yote kuteketea kwa moto.
Dereva huyo alisomewa mashtaka akiwa chini ya ulinzi wa polisi, anadaiwa kusababisha vifo vya watu sita barabara ya umma na kuendesha gari kwa mwendokasi na kusababisha abiria 17 kujeruhiwa.

Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Naima Mwanga, alidai mshtakiwa alitenda makosa hayo Julai 20, mwaka huu barabara ya Morogoro-Iringa , kwenye Hifadhi ya Taifa Mikumi, Wilaya ya Kilosa.

Mwanga alidai siku ya tukio saa 11:30 jioni katika hifadhi hiyo, akiwa dereva wa basi la Hood aina ya Scania, mshtakiwa anadaiwa kuendesha gari kwa uzembe na kugonga gari aina ya Semi Trela, mali ya Kampuni ya Frank Kefa, kisha kusababisha kifo cha dereva wa lori hilo, Bure Mayenga.

Shtaka la pili, anadaiwa kuua dereva msaidizi wa lori, Frank Kefa, ambaye ni mmiliki wa kampuni ya magari hayo.
Shtaka la tatu, siku na wakati huohuo anadaiwa kumuua kondakta wa basi hilo, Ibrahimu Shitindi, wakati shtaka la nne anadaiwa kumuua abiria wa basi, Joyce Kanikanila.

Mwanga alidai shtaka la tano, mshtakiwa anadaiwa kuumua abiria mwingine ambaye hakutambulika kutokana na kuungua na kubaki majivu. Shtaka la sita, anadaiwa kujeruhi James Shitindi, Peter Jamino, Elina Malekela na Joranda Mwasifiga.

Aliendelea kudai kuwa, mshtakiwa akiwa dereva wa mabasi ya Hood na mkazi wa Mbezi, alisababisha majeruhi kwa kuendesha gari kwa uzembe na hatari, ambao ni Leila Mgimwa, Amrani Salehe, Beatrice Mofuta, Rose Zambi, Jemina Ayuob na Richard Lubuvu.

Wengine waliojeruhiwa ni Theodory Raphael, Evance Mwasifiga, Benito Suga, Milk Maneno, Narropil Siroia, Kissa Mwakabuga, Asha Maneno na Charles Yesaya.Mtuhumiwa alikana kuhusika na tukio hilo na hakimu Janeth Kaluyenda, aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 10, mwaka huu itakapotajwa tena.

Kaluyenda aliahirisha kesi hiyo kutokana na mshtakiwa kusubiri kupelekwa Morogoro ili kufunguliwa mashtaka upya.

No comments:

Post a Comment