Tuesday, August 2, 2011

Mke auwawa na mumewe.



MKAZI wa Kijiji cha Namikango Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi, Aisha Philipo (28) amekufa, baada ya kunyongwa na mumewe katika ugomvi wa kugombea fedha zilizotokana na mauzo ya ufuta waliovuna kutoka shambani mwao msimu wa kilimo mwaka huu.

Habari kutoka wilayani humo na kuthibitishwa na vyombo vya Dola akiwemo Kamanda wa Polisi wa Mkoa, zinaeleza kuwa mwanamke huyo ameuawa, Ijumaa wiki iliyopita saa 12 jioni.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Sifuel Shirima alimtaja mwanamume huyo kuwa ni Hamidu Malibiche (31) ambaye pia ni mkulima na mkazi wa kijiji hicho cha Namikango.

Kamanda Shirima alisema siku ya tukio, mchana wanandoa hao waliuza ufuta wao na kujipatia Sh 90,000 alizokabidhiwa Aisha kuzitunza.

Alisema, ilipofika saa 12 jioni, mume alirudi nyumbani na kumuomba mke wake ampatie fedha hizo kwa malengo ya kuzitumia kinyume cha makubaliano, kitendo ambacho kilikataliwa na mwanamke huyo.

Akasema kitendo cha mwanamke huyo kukataa kuzitoa fedha hizo, kilisababisha ugomvi mkubwa hali iliyomfanya mwanamume huyo kumnyonga mkewe hadi kufa.

“Baada ya kitendo hicho cha mauaji, mtuhumiwa alijaribu kukimbia, lakini wananchi walifanikiwa kumkamata na kumfikisha Kituo cha Polisi,” alisema Kamanda Shirima.

Kamanda huyo alisema, mtuhumiwa kwa sasa anashikiliwa Kituo cha Polisi Wilaya ya Nachingwea na anatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya kukamilika kwa taratibu zikiwemo za upelelezi.

No comments:

Post a Comment