Wednesday, July 20, 2011
Report ya ajali ya HOOD.
WATU kadhaa waliokuwa wakisafiri jana kwa basi la Hood kutoka Mbeya kwenda Arusha wameteketea kwa moto huku wengine wakijeruhiwa vibaya baada ya basi hilo kugongana na lori lililokuwa limebeba mafuta ya kula kisha yote kuwaka moto.
Habari zilizopatikana kutoka katika eneo la tukio hilo zimesema ajali hiyo ilitokea majira ya saa nane mchana katika Barabara ya Morogoro - Iringa kilometa 20 baada ya kuingia katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.“Ajali hiyo ilitokana na moshi mkubwa uliosababishwa na moto uliokuwa umewashwa pembezoni mwa barabara,” mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Alex Kadeya alisema.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Joseph Rugila alisema mpaka anaondoka kwenye tukio saa 1:00 jioni, kulikuwa na watu watano ambao walikuwa wameteketea kabisa kwa moto.“Sasa niko njiani kurudi ofisini lakini mpaka naondoka, tulitoa mafuvu matano. Jumla ya watu waliofariki ni watano na majeruhi 41,” alisema.
Hata hivyo, alisema polisi bado haina taarifa kamili ya watu waliokuwa wakisafiri kwa basi hilo hivyo kushindwa kutaja idadi kamili ya watu waliopoteza maisha katika tukio hilo.
Lakini mfanyakazi wa Kampuni ya Mabasi ya Alsaedy, Jastine Joel ambaye alishiriki kuokoa maisha ya abiria hao alisema baada ya kufika katika Ofisi za Mwananchi, Dar es Salaam alisema idadi ya waliookolewa ni ndogo kuliko ya waliokuwa wamebaki ndani ya basi mchana huo.
“Lile basi lilikuwa na abiria 65 hivi na wafanyakazi watatu (dereva, kondakta na utingo), hivyo walikuwa jumla 68. Watu tuliofanikiwa kuwaokoa walikuwa 18 kabla ya moto haujakolea.”
Alisema basi lao liliwachukua majeruhi tisa wa ajali hiyo, watano kati yao akiwamo dereva wa basi hilo Salehe Tembo waliwaacha mjini Morogoro na wengine wawili walipakiwa katika basi jingine la Hood kuendelea na safari ya Arusha na wengine waliosalia waliwapeleka Dar es Salaam.
Joel ambaye basi lake lilikuwa limeongozana na basi hilo la Hood alisema: “Baada ya kugongana basi liliacha njia na kuelekea kwenye moto huku kichwa cha lori kikiwa kimeanza kuwaka. Mafuta yaliyokuwa yamepakiwa kwenye lori yalimwagika na kuongeza ukubwa wa moto.”
Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, John Shemkunde alisema wao ndiyo waliowasha moto huo ikiwa ni sehemu ya kawaida ya kuchoma baadhi ya maeneo ili kuweka mipaka na kuzuia madhara makubwa ya moto katika kiangazi.
“Tumekuwa tukifanya hivi miaka yote na hakuna ajali iliyowahi kutokea,” alisema Shemkunde alipoulizwa kama Hifadhi yake inastahili kubeba lawama kutokana na ajali hiyo kwa kutokuweka alama zozote za tahadhari wakati wa uchomaji huo.“Hapakuwa na haja yoyote ya kuweka alama. Ajali hii inaweza kuwa imesababishwa na uendeshaji mbovu.”
Watu wanaohofiwa kupoteza maisha katika ajali hiyo ni dereva wa lori, Bure Manyenga (50), mkazi wa Mbezi, Dar es Salaam na kondakta wake.Mashuhuda walieleza kwamba abiria waliopona ni wale waliobahatika kutoka nje ya basi hilo baada ya kuvunja vioo. Awali, Ofisa Upelelezi wa Mkoa wa Morogoro (RCO) Khamisi Suleiman alisema basi hilo lilikuwa na uwezo wa kubeba abiria 65. “Tunachojaribu kuangalia ni kuwa mpaka basi hili linafika hapa, (eneo la tukio) lilikuwa na watu wangapi ndani yake,” alisema Suleiman.
Hata hivyo, Mmiliki wa Kampuni ya Mabasi ya Hood, Mohamed Hood alisema basi hilo lilikuwa na uwezo wa kubeba abiria 60. Hakuweza kutoa taarifa zaidi akisema ametuma ujumbe kwenda katika eneo la tukio na hadi wakati huo alikuwa hajapata mawasiliano yoyote nao.
“Ajali ilipotokea nilikuwa nimetoka ofisini, baada ya kupata taarifa nilirudi na kuwatuma watu kwenda huko na mpaka sasa hawajanieleza lolote,” alisema.
Jitihada za Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji kujaribu kuzima moto huo hazikufanikiwa kiasi kwamba maiti zilizokuwa ndani ya basi hilo zilikuwa zikitolewa vipande vipande kutokana na kuharibika vibaya huku nyingine zikiwa zimeteketea kabisa kiasi cha kutoweza kutambulika.Ajali hiyo ilisababisha barabara hiyo kutopitika hivyo kuwapo kwa foleni na msongamano mkubwa wa magari.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment