Friday, February 4, 2011

Tamasha la Mwalimu Nyerere Feb. 14

TAMASHA la filamu la Mwalimu Nyerere linatarajiwa kuanza kurindima kuanzia Februari 14 hadi 19 kwenye viwanja vya Leaders Club, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi, Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF),
Simon Mwakifwamba, alisema ni mara ya kwanza kufanyika kwa tamasha hilo, ambalo litahusisha wageni kutoka Nollywood Nigeria, Afrika Kusini na Hollywood Marekani.
Alisema, siku hiyo ya ufunguzi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete atazindua rasmi TAFF sambamba na tamasha hilo, ambalo zaidi ya filamu 20 zilizofanya vizuri za ndani na nje zitaonyeshwa.
Aidha, Mwakifwamba alisema, mbali ya kuwepo kwa filamu hizo pia kutakuwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali likiwamo kundi la The African Stars ‘Twanga Pepeta’, FM Academia, Ambwene Yesaya ‘Ay’, Diamond, Khalid Mohamed ‘TID’, Mzee Yusuph, Lawrence Malima ‘Marlaw’, Albert Mangwea, Farid Kubanda ‘Fid Q’, Joh Makini na wengineo.
Aliongeza kuwa, katika siku za tamasha hilo kabla ya maonyesho ya siku husika, kutatunguliwa na mafunzo ya mada mbalimbali zinazohusiana na shughuli za filamu na maigizo kutoka kwa wakufunzi waliobobea.
Alisema, siku ya kufungwa kwa tamasha hilo, mgeni rasmi atatoa zawadi na tuzo kwa waasisi wa taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere na Rashid Kawawa ‘Simba wa Vita’ kwa mchango wao katika maendeleo ya taifa na tasnia ya filamu nchini.

No comments:

Post a Comment