Tuesday, January 18, 2011

Sifa 10 muhimu Mwanaume anahitaji mwanamke awe nazo!

NINA imani afya yako msomaji wangu ni njema na tayari umeshafungua ubongo wako tayari kwa kupata chochote kutoka katika safu hii muruwa kwa ajili ya kuwekana sawa katika uhusiano wetu.
Naam! Najua utakuwa umesherehekea vyema Sikukuu ya Pasaka na pilikapilika za kujitafutia riziki za kila siku. Karibuni marafiki zangu.

Somo ambalo bado linaendelea kushika hatamu katika ukurasa huu, ni kama linavyoonekana hapo juu. Sifa ambazo wanaume wengi wanapenda wanawake wawe nazo.
Rafiki zangu, kila mwanaume anayetaka kuoa, huwa na sifa ambazo anatamani sana mwanamke wake awe nazo, kila mmoja ana sifa tofauti ambazo itategemea na utashi wake, lakini tafiti mbalimbali zilizowahi kufanywa na Wanasaikolojia wa Mapenzi, wamebaini sifa 10 ambazo wanaume wengi wanapenda wanawake wawe nazo.

Katika majuma mawili yaliyopita, nilianza kwa kuanisha sifa 5, kwa faida ya wale ambao hawakubahatika kusoma ni pamoja na mwenye mapenzi ya dhati, anayeheshimu thamani yake, mwenye heshima, anayejitambua na aliye mfariji, sasa tuendelee na sifa nyingine.

5. Mkarimu
Wanaume wanapenda sana kuishi na wanawake wakarimu, ukarimu unahesabiwa kama sifa ya muhimu sana kwa mwanamke ambaye ana kiu ya ndoa. Ukarimu ni roho nzuri, huwezi kuwa mkarimu kama huna upendo, kukiwa na upendo ndani yako, hapo ndipo utakapokuwa na ukarimu.

Ukarimu utaanzia kwa mumeo kwanza, unakuwa naye karibu kwa kila kitu, kumuandalia chakula kizuri, kumpa pole akitoka kazini na hata kuwa mshauri wake anapokuwa na matatizo.
Hata hivyo, ukarimu hauishii hapo rafiki yangu, utatakiwa kuonesha ukarimu wako hata kwa rafiki zake wa karibu, mnapotembelewa na wageni nyumbani, lazima uoneshe ukarimu wako na upendo wa hali ya juu.

Inawezekana kwasasa bado mpo katika uchumba, lakini mara nyingi umekuwa ukienda nyumbani kwake kwa ajili ya kumfanyia usafi na kazi nyingine ndogondogo, rafiki zake wanapokuja, lazima uwakarimu.
Wapokee kwa upendo, watayarishie chakula au kinywaji, fanya kila unaloweza ili ukiondoka, wamweleze rafiki yao kwamba wewe ni mwanamke mwenye upendo na ukarimu. Dada yangu, ukiwa na sifa hii, utakuwa unajiweka jirani kabisa na ndoa. Tiba ya tatizo lako, ipo mikononi mwako mwenyewe.

4. Asiyehesabu makosa
Kukosea ni sehemu ya kujifunza, lakini inashauriwa kwamba mkosaji akigundua kwamba amekosea ni vyema akaomba radhi haraka. Katika mapenzi, kukosea ni kawaida na inawezekana mpenzi wako akawa anakosea mara nyingi sana, anakuudhi mara nyingi lakini anaomba msamaha.
Kuomba msamaha ni kujishusha, muungwana pekee ndiye anayeweza kufanya hivyo. Sasa kama mwenzi wako amekuomba msamaha, jifunze kusamehe kwa moyo, ukisamehe kwa dhati huwezi kukumbuka makosa, lakini ukisamehe kinafiki ni rahisi sana kukumbuka makosa ya mwenzako. Pointi kubwa hapa ni kwamba, hata kama mpenzi wako atakuwa amekukosea mara ngapi, kamwe usimkumbushe au kumsimanga kwamba amekuwa akikosea kila wakati.

“Kila siku wewe unakosea, mwezi uliopita ulinikosea, tena ukanipeleka mpaka beach kuniomba msamaha nikakusamehe. Hatujakaa sawa, ukakosea tena, ukalia chini ya miguu yangu, nikakusamehe.
“Wiki iliyopia tena ukafanya madudu yale yale na leo umerudia, wewe ni mpenzi wa aina gani, wewe ni mwanaume gani ambaye hauna msimamo? Kwa hili leo siwezi kukusamehe, kweli sitaweza!”

Kauli kama hiyo hapo juu si nzuri kabisa kwa mpenzi wako, unajua mara nyingi maneno mengi husababishwa na hasira, ukitulia hasira ikaisha¸unagundua kwamba hukuwa sahihi kutoa maneno fulani kwa mpenzi wako. Mtayazungumza yataisha, lakini ndani yake utakuwa umemwacha na funzo la mashaka, kwamba wewe si mwanamke sahihi kwake, jambo ambalo halitakuwa zuri. Sifa yako ya kuwa mke, utakuwa umeipoteza kuanzia hapo. Hakikisha una sifa hii.

3 Msaidizi
Upo msemo wa siku hizi, unasema; “Haki sawa kwa wote!” Huu ni msemo ulioundwa maalum kwa kutetea haki za wanawake. Wanataka haki sawa. Hakuna ubaya katika hili, lakini wanaume kwa kuzingatia msemo huo, siku hizi hawataki baba awe kila kitu nyumbani, mama awe msaidizi wa kweli.
Usaidizi ninaouzungumzia hapa ni kusaidiana majukumu mbalimbali ya familia, kwakuwa bado mpo katika uchumba, hutatakiwa kuwajibika sana katika mahitaji ya nyumbani kwake, lakini angalau ukionekana unachakarika na kazi yoyote, unakuwa umeingia kwenye cheni ya kuwa msaidizi wake wa baadaye.

Usichague kazi, bora iwe halali, jishughulishe ili uonekane siyo aina ya wanawake wale wanaopenda kuitwa ‘golikipa’. Hii ni sifa muhimu sana ambayo wanaume wengi wa sasa wanapenda wanawake wawe nazo.
“Kaka siwezi kuoa mzigo, mwanamke wa maisha yangu lazima awe anajishughulisha, kama hutakuwa makini, unaweza kuoa mzigo ambao hata chumvi ikiisha nyumbani atakubeep umpigie ili akuambie eti chumvi imeisha! Huu si uzembe?!” Anasema Roges (28) mfanyakazi wa Saluni moja ya kiume, Sinza ya Mori jijini Dar es Salaam katika mahojiano maalum nami hivi karibuni.
Umeona? Hapo ni kazi kwako kubadilika na kuhakikisha unakuwa na sifa hizo. Wiki ijayo tutamalizia sifa mbili za mwisho zilizosalia. Usikose.

No comments:

Post a Comment